RC” Mara ataka waliovamia eneo la hifadhi ya Serengeti kuondoka ndani ya siku 60
MKUU wa mkoa
wa Mara, Adam Malima, amewataka wananchi walioweka makazi na kufanya malisho
kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) kuondoka ndani ya siku 60
kabla hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa kwa wale waliofanya hivyo.
Akizungumza
na wananchi wa Kijiji cha Nyandage Kata ya Nyanungu wilayani Tarime mara baada
ya kutembelea vijiji vilivyo jirani nahifadhi hiyo,amesema sheria iliyopo
kuhusiana na masuala ya hifadhi lazima ifuatwe kwa kulinda rasilimali za taifa.
Amesema
ametumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe
Magufuli,pamoja na mambo mengine kusimamia sheria na hawezi kukubali kuona
sheria ikivunjwa kwa masrahi ya watu wachache.
Malima
amesema kazi iliyofanyika ya uainishaji wa mipaka imefanyika kisheria na mipaka
ya hifadhi hiyo ipo tangu mwaka 1968 na kuwataka wanasiasa wasitafute umaarufu
kupitia mipaka hiyo.
Amesema wapo
wananchi ambao
wamejenga na kuweka makazi ndani ya hifadhi na wengine kujenga
katika eneo la akiba la hifadhi jambo ambalo ni kinyume cha sheria na wananchi
wamekaa kwa mazoea.
Mkuu huyo wa
mkoa amesema mbunge wa jimbo
la Tarime vijijini, John Heche, ameongea sana
bungeni kuhusiana na jambo hilo ambalo limefanyika kisheria ambazo wamezitunga
wabunge na yeye ataendelea kuzisimamia kama zilivyo mpaka pale wabunge
watakapokaa tena na kuzibadilisha.
“ Kwa sasa
siwezi kwenda kinyume na sheria iliyopo,kwa yoyote ambaye ameweka makazi ndani
ya hifadhi na kwenye eneo la akiba natoa siku 60 kila muhusika aweze kuondoka.
“ Kiongozi
wangu wa chama Mwenyekiti wa wilaya(CCM) naye amejenga na kufanya shughuli za
malisho katika eneo la akiba la hifadhi nimemwambia aondoke ndani ya siku 60
nilizozitoa ili tulinde hifadhi zetu,”amesema Malima.
Mhifadhi wa
kanda ya kaskazini katika hifadhi hiyo ya Serengeti, Lameck Matungwa, amesema
kazi ya uainishaji mipaka wameifanya kwa mujibu wa sheria ili kuweza kulinda
mipaka na sivinginevyo.
Amesema ni
aibu kuona nchi jirani ya Kenya katika eneo la hifadhi ya Masai Mara likilindwa
na kuzuia uingizaji wa mifugo kufanya malisho lakini kwa Tanzania imekuwa ni tofauti
na kuwafanya wahifadhi kufanya kazi ya kupambana na mifugo
Mhifadhi wa Kanda ya kaskazini katika hifadhi ya Serengeti,Lameck Matungwa, akizungumza na Waandishi wa Habari |
Mkuu wa wilaya ya Tarime, Gloriois Luoga, akisisitiza jambo wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa kwenye hifadhi ya Serengeti |
Zizi la Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tarime, Daud Ngicho,lililojengwa ndani eneo la akiba la hifadhi
Nyumba ya Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tarime ambayo imejengwa kwenye eneo la akiba la hifadhi ambapo mkuu wa mkoa ametoa siku 60 wavamizi wote kuondoka hifadhini
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tarime,Daud Ngicho, akilia baada ya kuambiwa kuondoka eneo la hifadhi
Mhifadhi Matungwa(kushoto) akiwa na mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu
Nyumba ambazo zimejengwa kwenye eneo la akiba la hifadhi
Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima
akisisitiza jambo
Mhifadhi akimuonyesha mkuu wa mkoa wananchi walioingiza mifugo hifadhini
Mifugo ikiwa ndani ya hifadhi
Mwananchi akichunga hifadhini
Mkuu wa mkoa akiwa eneo la hifadhi
Msisitizo juu ya kuhama eneo la hifadhi
No comments